SOKA AFRIKA: Yanga SC jogoo la shamba

Dar es Salaam. Waswahili  husema, jogoo la shamba haliwiki mjini. Hicho ndicho kinachoweza kusemwa wakati Yanga ikikabiliwa na kitendawili kigumu inachotakiwa kukijibu kesho kwenye Uwanja wa Olympique de Sousse  (saa 3 usiku kwa saa za Tanzania).
Ikiwa na rekodi ya ubingwa mara 25, Yanga itashuka uwanjani kuikabili Etoile du Sahel, Tunisia katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa hao wanahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kusonga mbele katika mashindano hayo.
Hata hivyo,  wakati Yanga ikijiandaa kuikabili Etoile, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa tangu mwaka 2006, watoto hao wa Jangwani wamekuwa na matokeo mabaya ugenini kuliko nyumbani katika mashindano ya kimataifa, ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Gazeti hili  limebaini kuwa Yanga katika michezo 16 iliyocheza ugenini tangu 2006 imeshinda miwili dhidi ya klabu mbili za Comoro na kupoteza michezo 13, wakati mchezo mmoja ikipata ushindi wa mezani.
Yanga iliiifunga Etoile d’Or ya Comoro, mabao 6-0 ugenini mwaka 2009 katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabla ya hapo, Yanga ilishinda nyumbani kwa mabao 8-1 na hivyo kusonga mbele kwa kuifunga timu hiyo mabao 14-1.
Pia, ilishinda ugenini mwaka 2014 katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Komorozine ya Comoro kwa  mabao 5-2.
Awali, nyumbani Yanga ilishinda kwa mabao 7-0 na hivyo kuiondosha timu hiyo kwa mabao 12-2.
Timu hiyo  ilipata ushindi wa mezani, ugenini mwaka 2007 katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya wapinzani wao,  AJSM ya Madagascar kujitoa baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na wao kufungwa  mabao 5-1.
Ukiondoa michezo hiyo, Yanga imefungwa mechi nyingine zote ugenini.
 Pamoja na msimu huu kuwa na kikosi bora na safu imara ya ushambuliaji, ikiwa  imefunga mabao 51 katika michezo 24 ya Ligi Kuu,  bado timu hiyo imeshindwa kutamba ugenini.
Mwaka huu katika Kombe la Shirikisho, Yanga ilianza kutoa dozi kwa BDF XI ya Botswana kwa kuichapa mabao 2-0, nyumbani na kisha kufungwa ugenini 2-1 na kusonga mbele kwa ushindi wa wa mabao 3-2.
Katika mchezo dhidi ya  Platinum ya Zimbabwe, Yanga ilishinda mabao 5-1 nyumbani, kabla ya kunyukwa bao 1-0 ugenini na kusonga mbele.
ADVERTISEMENT
Jinamizi la kufanya vibaya  kwa Yanga ungenini limeanza siku nyingi, kwani ukiangalia  mwaka 2006 kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,  timu hiyo ilishinda nyumbani dhidi ya Zanaco ya Zambia kwa mabao 2-1, lakini ikafungwa ugenini mabao 2-0 na hivyo kutolewa kwa mabao 3-2.
 Kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2007 baada ya AJSM Madagascar kujitoa na Yanga kupata ushindi wa mezani,  timu hiyo iliikabili Atlético Petroleos Luanda ya Angola na Yanga kushinda nyumbani kwa mabao 3-0, lakini ikaja kulala ugenini kwa mabao 2-0, hata hivyo ilifuzu kwenda hatua  ya pili.
Katika hatua ya pili,  Yanga ilipambana na  Esperance ya Tunisia na kufungwa mabao 3-0 ugenini na kisha kutoka suluhu nyumbani. 
Kwenye  Kombe la Shirikisho katika mwaka huo, Yanga ilijikuta ikishia katika hatua ya 32  baada ya  kutoka suluhu  na Al-Merrikh ya Sudan nyumbani na kisha kufungwa mabao 2-0 ugenini.
Pia, Yanga ilishinda katika hatua za awali za Kombe la Shirikisho mwaka 2008 baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini kutoka kwa AS Adema ya Madagascar,  lakini ikashinda nyumbani kwa mabao 2-0 na hivyo kuvuka raundi nyingine kwa mabao 2-1.
Kwenye hatua ya 32 ya Kombe la Shirikisho mwaka 2008, Yanga  ilitoka sare nyumbani ya bao 1-1 Al-Akhdar ya Libya, ikanyukwa ugenini kwa bao 1-0.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2009, Yanga ilishinda hatua ya  awali kwa kuichapa Comoro,  jumla ya mabao 14 -1 katika mechi ya nyumbani na ugenini, lakini ikakutana na kigingi baada ya kukutana  na Al-Ahly ya Misri kwenye raundi ya kwanza na kuchapwa mabao 3-0 ugenini baada ya kupigwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2010,  kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilikubali kipigo nyumbani cha mabao 3-2 dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya DR Kongo,  lakini pia ikafungwa ugenini bao 1-0.
Pia, ikatolewa kwenye raundi ya awali ya  Kombe la Shirikisho mwaka 2011 na Dedebit ya Ethiopia baada ya kutoka sare ya mabao 4-4 nyumbani na kisha kufungwa mabao 2-0 ugenini. Timu hiyo ilitolewa tena katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2012 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Zamalek ya Misri,  lakini ikalala ugenini kwa bao 1-0.
Baada ya mwaka huo, Yanga haikushiriki michuano ya kimataifa mwaka uliofuata baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara.
Mwaka 2014, Yanga ilishiriki tena michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanikiwa kuvuka hatua ya awali baada ya kuifunga Komorozine ya Comoro jumla  ya mabao 12-2, ikishinda nyumbani mabao 7-0 na ugenini 5-2.
Baada ya hapo ikakutana tena na  Al Ahly ya Misri na kushinda nyumbani bao 1-0 na kisha kulala ugenini kwa bao 1-0 na mchezo huo kwenda katika matuta na Al Ahly  ikashinda kwa penalti 4-3.
Yanga ikakutana na Etoile du Sahel ya Tunisia jijini Dar es Salaam na kutoka nayo sare ya bao 1-1 na sasa kinachosubiriwa ni mchezo wa marudiano kesho ili kujua  kama itaweza kuvuka na kuendelea na hatua nyingine au la.
Tusubiri tuone, ingawa rekodi zinaisuta.
POSTED FRIDAY, MAY 1, 2015 | BY- OLIVER ALBERT, MWANANCH
Powered by Blogger.