UHAKIKI WA USHAIRI WA KISWAHILI



UHAKIKI WA USHAIRI
KITABU: KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI GORA HAJI
WACHAPISHAJI: TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani inayozungumziwa juu ya mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja na suala zima la ujenzi wa jamii mpya. Katika diwani hii, mwandishi ametoa maadili na maonyo mbali mbali pamoja na mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii hapa nchini.
Maudhui
Dhamira Kuu- Ujenzi wa jamii mpya
    Mwandishi amejadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya katika kazi yake. Katika diwani hii mwandishi ameonesha vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini. Vikwazo hivyo ni kama vile uongozi mbaya, rushwa,  tamaa, ukosefu wa elimu, ukoloni mamboleo, n.k.
     Katika kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia  mbalimbali ambazo  jamii inapaswa kuzitumia  katika zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
1.     Uongozi Bora
     Mwandishi ameonesha kuwa Uongozi bora  unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta ufanisi mzuri katika utendaji na utekelezaji wa  majukumu mbalimbali kwani  Uongozi mbaya unasababisha kushindwa kufikia malengo. Kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana jamii hufikia kufanya mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika uongozi mpya ili kuijenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi  anaongelea juu ya mapinduzi yanayofanywa na tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala.mwandishi anasema;
‘’kimbunga mji wa siyu,kilichowahi kufika,
Si kwa yule wal huyu,ilikua patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika.
 Ametumia mji wa Siyu kama kielelezo kizuri kwa jamii  yoyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi wabovu na kuleta viongozi bora. Katika mapinduzi hayo mwandishi amefafanua kuwa wengi ndio wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi la “Madanganyo linazungumzia jinsi uongozi mbaya unavyowadanganya wananchi, unavyowaathiri na kuwakera wananchi. Wananchi hushiriki katika shughuli za uzalishaji mali (miradi mbli mbali) lakini matunda ya jasho lao hufidiwa na wachache. Wachache hao husahau wale waliosulubika katika uzalishaji na mtokeo yake wnanchi wanaishia kuishi maisha ya taabu. Ubeti wa 6, msanii/mwandishi ansema;
“Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, kwa mapanga na mshoka,
Manufaa kwa wakuu, wadogo yetu mashaka,
Wezeni kutukumbuka, mjue nasi wenzenu.”
Shairi la “Wenye Vyao Watubana” (uk 8) mwandishi amejadili namna matajiri  au vitu jinsi wanavyowagandamiza, kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote. Mwandishi anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii. Hii ni kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi hawachukui tahadhari.Ubeti wa 7, mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga, kwa lochi wa darajani,
Kujitole mhanga, kwa bei hiwezekani,
Mvao wake wa kanga, ni shilingi elifeni,
Wakubwa tuteteeni, wenye vyao watubana.”
Shairi la “Kibwangai linajadili dhana ya usaliti wa viongozi wetu kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi wanavyowachagua viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au wakishashika nyazfa wanageuka na  kuwasaliti wananchi waliowachagua. Msanii anathibitisha hayo kwenye ubeti wa 7;
Kibwangai alipoona, ni mtu kakamilika,
Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya,
Wala hakujali tena, wenzake waliwambiya,
Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu.”
Shairi hili, limetumia taswira ya Kibwangai  kuwakilisha viongozi wasaliti na nyani kuwakilisha wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai yaani watawaliwa.
Katika shairi la “Hili Mnatutakiya” , mwandishi anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi ,jeshi namna  vinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na kuwashughulikia wahalifu..Ubeti wa  1msanii anasema;
 Twasema kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu mkatubwaga,hasa ukiangaliya,
Hao wezi mwafuga,wazidi kutuibiya,
      Msanii ameonesha kuwa vyombo hivyo ndivyo  vinavyowalinda wezi,majambazi na matapeli.Kwa ujumla  msanii wa  diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
2.      Kupiga vita rushwa 
Rushwa ni kikwazo kimojawapo kinachokwamisha kujenga  jamii kwa upya. Kutokana na rushwa kuota mizizi  katika jamii haki hupotea, wachache wanafaidi matunda ya nchi  na wengine wanaendelea kuumia. Shairi la “Rushwa”   mwandishi anasema;
Rushwa kajenga kambi, na kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi, mkaidi hashindiki,
Tumzushieni wimbi, isiwe kutahiliki,
Tumchimbie handaki, rushwa tukamzikeni.”
      Katika ubeti huu, mwandishi anatuonesha kuwa lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki na usawa vitawale.Kupiga vita rushwa ni njia pekee itakayoisaidia  kujenga  jamii mpya ambayo mwandishi ameipendekeza.
3.      Umuhimu wa Elimu
       Ili tuijenge  jamii mpya ni lazima watu wapate elimu na waelimike bila kujali umri. Mwandishi anawahimiza wazee kujiunga na kisomo chenye manufaa ili wafute ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.  Mwandishi anathibitisha haya katika shairi la “Kisomo cha Maarifa  Msanii ansema;
Kisomo chenye manufaa,tusomeni kwa haraka,
Isiwe tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
katika shairi hili mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu wazima kwa sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya maendeleo. mwandishi anaonesha kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya kwani  bila kuwa  na wasomi katika jamii kama hii yetu zoezi la ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
4.      Kupiga vita ukoloni mamboleo
Ukoloni mamboleo ni kitendo cha nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini kimaamuzi inatawaliwa na nchi nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya uchumi hapa nchini. Na ili tuweze kufanikisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini hatuna budi kupiga vita ukoloni mamboleo . Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi anaonesha jinsi ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa chini. Ukoloni mamboleo unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na kuwasetiri matajiri au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
Ambao ni matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri, salama kujipatiya,
Walokuwa mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye Chuwi gani?
Mwandishi ameeleza kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi zinazoendelea. Hivyo mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia) hizo na tuupinge ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii mpya.
5.      Umuhimu wa kujitawala
Ili tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja  zote za kifikra, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “ Mwandishi anaeleza kuwa ili tuweze  kujitawala ni lazima tuepukane na unafiki, vibaraka (wasaliti),  tusikate tama na tudumishe amani.  Katika ubeti wa 3 msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe, wasio wenye kuzuzuka,
Tamaa uwakalishe, yasiwe unayotaka,
Katu wasiwawezeshe, wabakie kuzuzuka,
Katu washindike mahusuda, wasiopenda bara letu.”
Katika shairi la “Kujitawala”  Mwandishi anaeleza  umuhimu wa  kujitawala kwa jamii yoyote ile. Mwandishi anaonesha kuwa, kujitawala ni pale umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa au kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa 1 Msanii anasema:-
Kujitawala ni kwema, kuliko kutawaliwa,
“Kujitawala ni umma, kila yao kuamua…”
Katika shairi hili la kujitawala mwandishi anonesha faida mbalimbali za kujitawala kama vile demokrasia, kuwepo umoja naushirikiano, kuwepo haki na usawa, amani hudumishwa, vile vile mila na desturiza nchi zinadumishwa. Hivyo mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tujitawale kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra.
6.     Umuhimu wa kazi na kuwajibika
Kazi ni nguzo muhimu  sana ya ujenzi wa jamii mpya. Mwandishi amesisitiza umuhimu wa kazi na kuwajibika katika shairi la “Kazi”  Mwandishi anatuonesha kuwa kzi ndio msingi wa maendeleo. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na tuepukane na uvivu. Ubeti wa 1, mwandishi anasema;-
         “Pesa huletwa na kazi, ni njia zipitiayo….”
   Katika shairi la “Uokolewe”, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano ili kuuinua uchumi wetu. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa  bidii kutumia vyema  rasilimali zetu za kuinua uchumi wetu. Hivyo  msanii aniasa jamii kujihusisha na ukulima, uvuvi, utalii na viwanda ili kujenga jamii kwa upya.
      Katika shairi la “Dumizi mwandishi anakemea  tabia ya baadhi ya watu kukaa bila kazi (uvivu) na kuanza  maisha ya kunyonya. Hivyo mwandishi anapiga vita unyonyajiwa watu waishio kwa jasho la wenzao.
7.     Mapenzi na ndoa
    Katika diwani hii, mwandishi ameonesha kuwa mapenzi yamegawanyika katika pande kuu mbili ambayo Kuna mapenzi ya kweli na udanganyifu.
    Katika shairi la “Usimpige Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga mke wake na vile vile  mwanaume hatakiwi kumwekea mkewe masharti magumu.
    Shairi la “Hongera mwandishi anaendelea kujadili suala la mapenzi na ndoa katika jamii zetu. Anawaonya wanandoa(bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana wawapo nyumbani. Amewapa kila mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za  (4-5) mwandishi anasema:-
4- “Bi arusi yangu shika, uyatie akilini.
       Mumeo akifika, anapotoka kazini,
       Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
        Hongera.”
5- “Bwana arusi sikia, ukiwa kwako nyumbani,
        Maneno ya kutupia, hayafai asilani,
         Kauli njem tumia, na lugha iwe laini,
         Hongera”
Katika shairi la “Sifa ya Mke” Msanii  anaonesha kuwa sifa kubwa ya mwanamke ni tabia na wala  si sura. Sifa ya tabia njema humpa mwanamke taadhima, huruma, utiifu na hata uhodari. Anaeleza kuwa  mwanamke anapaswa kuwa  mtulivu, asiwe kiruka njia, asiwe na ufedhuli wa aina yoyote, uovu, n.k.
Katika shairi la “Sitaki  Mwandishi anakemea mapenzi ya udanganyifu yaliyoshamiri katika jamii zetu kwa wakati huu. Anasema:-
Rabi simpe mapenzi, hakuna wa kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi, ni wachache duniani,
Mapenzi yamepotea, sasa ni adimu sana,”
Ni kweli mapenzi ya siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina pamoja na udanganyifu.
8.     Maonyo na maadili mema katika maisha
 Mwandishi amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu kuhusiana na harakati mbali mbali za maisha. Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni kielelezo kizuri kinachofaa kufuatwa na kizazi hiki. Maadili na maonyo haya ni ya muhimu sana katika maisha. Maadili hayo ni kama vile:-
(a)Malezi bora katika jamii ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msingi bora wa maisha. Katika shairi la “Vijana wa Zanzibar” Mwandishi ameonesha kuwa matendo ambayo vijana wa siku hizi  wanayatenda si mazuri, ni ya kusikitisha.  vijana wa siku hizi hawana utii, ni wajeuri, ni wadanganyifu, ni majambazi na pia hudharau mila na desturi zetu za asili a kukimbilia tamaduniza kigeni. Katika  ubeti wa 2 msanii anasema:-
Mwawacha yenu ya hapa, ambayo yako mazuri,
Kutii na kuogopa, mwaona haina heri,
Mwayavamia kwa pupa, kwa kedi na jeuri,
Mila zetu za fakhari, wacheni kuzipotosha.”
  Kulingana na ubeti huu,mwandishi anaonesha kuwa suala la malezi bora ni muhimu sana katika jamii ili kuwaandaa vijana wetu kuendana na mazingira wanamoishi.
.
Kwa ujumla, katik suala la malezi mwandishi anaifundisha jamii kuwa, samaki mkunje angali mbichi.
b)Umuhimu wa kuwathamini wazazi  
Mwandishi ameonesha kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi. Katika shairi l “Wazazi ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao ya mtoto; mtoto hatakiwi kuwakasirikia, kuwaudhi wala kuwachikiza bali anatakiwa kuwa na mapenzi nao. Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni  kumpa chakula, mavazi, malezi mema pamoja na elimu. Katika ubeti wa 4:-
Wakatafuta walimu, kukupatia ujuzi,
Wakakufunza elimu, pamoja na matumizi,
Sasa ni mtu timamu, waendelea na kazi,
Usiwaudhi wazazi, hiyo ndiyo yako ngao 
Katika shairi la “Ulezi Kazi” Mwandishi ameonesha jinsi mama (wazazi) wanavyohangaika kubeba mimba hatimye kuzaa na kuanza kazi ya ulezi wa mtoto hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Anaonesha kuwa wazazi hupata taabu na shida mbalimbali katika ulezi wao. Hivyo mwandishi anashauri wazazi wathaminiwe napewe heshima zote.
c)Kuepukana na umbea
Umbea ni ile tabia ya kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii si nzuri, kwani huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika shairi la “Wacha Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na badala yake ijishughulishe katika shughuli za uzalishaji mali. Madhara ya umbea ni kama vile majungu, uchochezi,  n.k. Umbea pia husababisha utengano. Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Wacha kupika majungu, na kuleta uchochezi,
Kuwajaza walimwengu, kasumba zile na hizi,
Hicho kimoja kifungu, huletesha ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi, huvunja mafanikio.”
Katika shairi la “Hayafai Mitaani mwandishi anaionya jamii kuwa si jambo la busara au zuri kusambaza au kupeleka taarifa ya jambo fulani sehemu ambayo haihusiki. Anaona kuwa ni busara sana endapo jambo fulani limefanyikia sehemu fulani liishie huko huko lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu isiyohusika. Si tabia nzuri kupeleka mitaani kwa watu wasiohusika. Ubeti wa 2 unasema:-
Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani, mitaani kufikisha,
Kwani siri ya mwituni, si vyema kuelewesha,
Ya kunini huishia kunini.”
Hivyo mwandishi anatushauri kuwa jambo mojalikitendeka sehemu moja ni bora liishie katika sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
(d)Kuepukana na udokozi (tabia ya wizi)
Udokozi ni ile hali ya kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au kunyang’anya. Mwandishi anakemea tabii hii kwani  si nzuri. Tabia hii ipo miongoni mwa wanajamii. Mwandishi anaonya kuwa tabia hii huhatarisha maisha ya wahusika yaani wenye tabia hii. Mwandishi amemtumia paka kuwakilisha watu wenye tabia hiyo. Aidha mwandishi anaendelea anaelezea  kuwa tabia hii husababisha uchokozi, ugomvi  pamoja na chuki katika maisha.
(e)Umuhimu wa shukrani katika maisha
Mwandishi anaieleza jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu mwingine. Katika shiri la “Punda mwandishi ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo na shukrani katika maisha . Ameonesha kuwa mwandamu asiye na shukrani hata umfanyie wema kiasi gani hawezi kutoa shukrani. Ameelezea kuwa mtu asiye na shukrani ni kuachana naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa. Anasema;
Punda hakumbuki wema, hta kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na majianufaike,
Katu hawi salama, shukrani zake mateke,
Ndiyo tabia ya punda, kurusha rusha matee,
Kuchunga akikushinda, mwacheaende zake.
Katika ubeti huu, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa fadhila.
UJUMBE
-Dhana potofu ya kudhani bila ya kuwa na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa sababu hupotosha ukweli wa mambo
-Mapenzi na ndoa ya dhati ni muhimu katika jamii zetu
- Ukoloni mamboleo, uongozi, mbaya, rushwa na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
- Maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.

FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msimamo na  mwendo bora wa maisha na anatetea misingi ya haki na utu katika jamii.
MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo katika jamii kwa kudhani tu bila kuwa na misingi ya kisayansi.
FANI
a)Muundo
Mwandisha ametumia miundo tofauti katika diwani hii kma vile;Tarbia (mistari 4), Tathlitha (mistari 3) katika shairi la “Kujitawala” (uk 7-8).
    Pia ametumia muundo wa takhimisa  (sabilia) – mistari 5 na kuendelea katika shairi la “Punda” (uk 21-22), shairi la “Bahati” (uk 36).
b)Mtindo
Mtindo uliotumika ni ule unaofuata kanuni za mapokeo za urari wa vina na mizani pamoja na mpangilio wa beti. Karibu mashairi yote yana vina vya kati na mwisho isipokuwa katika mashairi ya “Kimbunga” (uk 1), “Dumuzi” (uk 41), “Madereva” (uk 43), “Chuwi” (uk 42) yana nusu mstari katika kituo.
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi ametumia lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja  yenye mafumbo na taswira mbali mbali na tamathali za semi kidogo na misemo kwa kiasi.
d)TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
-Kwenye shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
-Ufedhuli na uovu kama yake mazoea.
-Awe kama malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi ametumia mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali, machafu, matusi kw kutumia tafsida. Mfano shairi la “Nyang’au” (uk 44) linahusu tamaa, “Paka” (uk 22) linahusu wizi, shairi la “Dumuzi” (uk 41) linakemea uvivu, n.k.
Mbinu Nyingine za Kisanaa
Takriri
Mwandishi ametumia takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8) neno kujitawala limerudiwarudiwa.
Matumizi ya Taswira
Mwandishi ametumia taswira nyingi kama vile;
Mfano: Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
          Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi wasaliti
          Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi waliosalitiwa
         Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni mamboleo, n.k.
Jina la Kitabu
Jina la Kitabu Kimbunga halisadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili katika kitabu hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya kimaisha. Asilimia kubwa ya mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo na maadili katika maisha.
Kufaulu kwa Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu
-Kutoa maadili mema na maonyo katika jamii
- Kujadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya
-Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani
-Ametumia lugha rahisi, mafumbo, taswira, n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
--Baadhi ya maadili aliyoyajadili katika kitabu hiki ameyajadili kidhanifu, ni sawa na yale tunayoyapata makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii mpya
-Vile vile amejadili masuala mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu. Kama vile maswala ya kipaji (uk 38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani
v Mwandishi ametumia  lahaja ya Unguja badala ya Kiswahili sanifu ivyo ni vigumu  kueleweka kwa watu wote.
v Diwani hii ni ya hali ya chini sana katika muundo, mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya kisanaa.

UHAKIKI WA USHAIRI
KITABU: FUNGATE YA UHURU
MWANDISHI: MOHAMED S. KHATIBU
WACHAPISHAJI: DUP
MWAKA: 1988
UTANGULIZI
    Fungate ni kipindi cha siku saba baada ya harusi..Ni kipindi ambacho Bwana na bibi harusi hula na kunywa tena milo ya kuchagua wakati wote wa fungate.Fedha na vifaa vitumiwavyo na maharusi huwa ni vya kuazima au kuchangiwa(si lazima viwe vyao) Wanapewa  kutoka kwa ndugu na jamaa na hata na vijana wa kuwahudumia.Wachangaji hufanya hivyo kwa sababu wanajua kuwa fungate ni ya muda mfupi(siku saba tu),hivyo huvumilia.
Fungate ni lazima iwe na kikomo.Ikizidisha kikomo hicho ibadili jina labda iitwe unyang’anyi,ulimbwende,uvivu,uzembe au jina lolote lenye kashfa hasa unafiki au usaliti.Mwandishi wa diwani hii ameimwaga ghadhabu hiyo kwa hao maharusi waliohesabu ukarimu wao kuwa ni upumbavu.
Uhuru:Uhuru ni neno linalopendwa sana na wanasiasa wa ubepari au ujamaa.Hekaheka za uhuru(kudai,kuomba au kupigania) zinaweza kufananishwa na shughuli za kutafuta mchumba,kupeleka posa kulipa mahari,na kufunga ndoa.
Katika kipindi chote cha uhuru, watu, hususani viongozi,hufurahi na kufanya sherehe ambazo huwagharimu raia-mali na vitu mbalimbali.Lakini kwa kuwa uhuru ni kitu cha thamani kama maharusi,raia hukubali kugharimia sherehe hizo.Lakini pia sherehe za uhuru kama fungate hutazamiwa iwe ya muda mfupi –labda mwezi  mmoja au miwili.
Raia wanchi zilizopata uhuru barani Afrika walikuwa na shauku ya kupata maendeleo lakini hawajafikia lengo lao hadi sasa kwa sababu viongozi wetu wanaendeleza Fungate ya Uhuru.Hivyo viongozi wanchi za Afrika wamewasaliti wananchi wao waliowachagua.Katika utangulizi mwandishi anasema ;
Nikate tama,
Kwani tuendavyo,hatufiki,
Vile ipasavyo,hayakamiliki,
Mambo yalivyo,ni unafiki,
Tumesalitiwa!
MAUDHUI
    Fungate ya Uhuru ni diwani inayojdili kwa mapana sana juu ya matatizo mbalimbali yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa Tanzania.Matatizo hayo ni kama vile usaliti,unafiki,wizi,hujuma,udanganyifu,rushwa pamoja na uongozi mbaya.

Dhamira Kuu: Ujenzi wa jamii mpya.
Mwandishi anajadili kwa kiasi kikubwa suala la ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi anaitaka  jamii  itupilie mbali unyonyaji , uonevu, dhuruma, udanganyifu, wizi, unafiki,  umasikini, uongozi mbaya na ukandamizaji wa watu wa tabaka la chini ili kuijenga jamii kwa upya.Jamii ambayo hatamu zote za uongozi (utawala,siasa na uchumi) zitakuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi kwa misingi ya haki na usawa.
     Itikadi ya kujenga jamii mpya ilijengeka juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilitangazwa mwaka 1967 baada ya kutangazwa kwa  Azimio la Arusha.Hadi 1988,mwandishi anaandika kitabu hiki anaonesha kuwa bado hatujafanikiwa kujenga jamii mpya hapa Tanzania.Hii inatokana na sababu zifuatazo;
  Kwanza,bado kuna dhuruma, usaliti,unyonyaji na wizi wa mali za umma.katika  shairi la “Wingu’’  mwandishi anasema;
Bado:
Wingu limetanda,
Limetanda,
Na kutughubika ghubi,
Mvua:
Lakini hainyeshi,
Hainyeshi,
Ukame umetanda waa!
Mimea:
Tulipanda kwa miongo,
Kwa miongo,
Yote imekauka!
Pia katika shairi la “Wizi”mwandishi ameonesha dhahiri kuwa wizi umo ikuluni, bomani, kanisani, misikitini, na hekaluni.Mwandishi ameonesha kuwa dini zawabariki wezi, polisi hulinda wezi, na majeshi huhalalisha wizi.katika ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Wizi umo;
  Kanisani,
Msikitini,
Kasirini,
Na bomani,
Wanyang’anywao ni waumini.
Pili, mwandishi ameonesha kuwa bado kuna matabaka katika jamii zetu.Ameonesha kuwa kuna tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho.Tabaka la juu (utawala) unaolinyonya tabaka la chini(tawaliwa).Mfano katika shairi la “Fungate” mwandishi ameonesha jinsi tabaka tawala linavyofurahia maisha kwa kuishi katika majumba mazuri, kutembelea magari ya faharin, n.k.
Katika shairi la”Waja wa Mungu”mwandishi anaonesha jinsi tabaka la chini linavyoishi kwa shida.Kwa mfano, kula kwa shida, kulala kwa shida, kuvaa kwa shida, hawapati elimu na huduma nzuri za afya.
Tatu, mwandishi ameonesha kuwa, bado kuna uongozi mbovu katika jamii zetu.Mfano katika shairi la “Viongozi wa Afrika” mwandishi anashutumu vikali viongozi wanaotumia  madaraka  yao  vibaya na kugandamiza watawaliwa.Anasema;
Viongozi wa Afrika,
Wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,
Wao wachache na werevu,
Na umma wote ni mpumbavu,
Wanafiki,
Wazandiki”.
Pia shairi la “Njama”  mwandishi anaonesha  jinsi viongozi wanavyotumia njama mbalimbali kulinyonya tabaka tawaliwa.Viongozi wanatumia njama mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hakuna anayewapinga wala kuhoji hata kidogo.
   Nne, mwandishi anaonesha kuwa, kuna unyonyaji wanaofanyiwa wakulima katika kuuza mazao yao.Ameonesha kuwa wakulima hunyonywa na kudhurumiwa na kupewa bei kidogo wakati kuuza mazao yao.Shairi la “Naona”mwandishi  linadhihirisha haya katika ubeti wa 6,ansema;
   Naona
  Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
      Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge ulele.
       Ni kutokana na matatizo hayo ya wizi, rushwa, uongozi  mbovu, dhuruma, uonevu na unyonyaji ndiyo maana tumeshindwa kujenga  jamii mpya.
Mwandishi ameonesha mbinu mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia ili  kuijenga   jamii mpya na hizo ndizo  dhamira ndogo ndogo za diwani hii kama zifuatazo;
1.Kuwa na uongozi bora
 Uongozi mbaya ni kikwazo kikubwa  katika ujenzi wa jamii mpya.Shairi la”Fungate” Mwandishi ameonesha jinsi viongozi wanavyotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyonya wananchi wa kawaida.katika ubeti wa 1 mwandishi anasema;
  Fungate ya uhuru,bado inaendelea,
“Harusi” wana nuru,wazuri wanavutia,
  Wengi inawadhuru,na tena wanaumia
     Mwandishi anaeleza kuwa tangu tupate uhuru hadi leo bado viongozi wetu wapo Fungate wakila na kunywa huku wananchi wakiendelea kuteseka na maisha magumu,hivyo mwandishi anaitaka jamii kuung’oa  uongozi mbaya na kusimika uongozi uliobora unaowajali wananchi wake .
Shairi la “Viongozi wa Afrika”mwandishi anakemea viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kujinufaisha wao wenyewe, wenye hisa katika viwanda, mabenki, makampuni au mashamba ya mabepari kuwa ni wasaliti.Anawakemea wale viongozi wenye upendeleo, wanaotumia pesa za umma kwa kuendeshea sherehe.Mwisho anawakemea viongozi wanaopokea rushwa na amewaita magaidi au mafisadi.
  Shairi la “Utawala” mwandishi amehimiza kuuangusha utawala wa kibepari ambao unawanufaisha wachache na walio wengi hunyonywa, hugandamizwa, huonewa na kunyanyaswa na hao wachache.
Shairi la “Kinyang’anyiro” mwandishi anaonesha jinsi viongozi walivyokimbilia kushika madaraka (hasa enzi za uhuru) lakini wanashindwa kuleta maendeleo hapa nchini.
    Kwa ujumla mwandishi anapendekeza kuwa, ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora .


2. Kuwa na umoja na ushirikiano
Mwandishi anaona kuwa  ili  tujenge jamii mpya ni muhimu tuungane  sote tuwe kitu kimoja “Katika shairi la “Unganeni” mwandishi anawataka wananchi wote wa Afrika kuungana ili kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa. Anasema:-
Wafanyakazi wa Afrika, tuungane,
Na wakulima kadhalika, tushikamane,
Makabwela  mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa mapambano, yalo marefu,
Ushindi ni wetu”.
   Mwandishi anaitaka jamii hasa tabaka la chini kuungana na kuendeleza mapambano dhidi ya viongozi wanafiki, mabepari, mamwinyi wanaonyonya, wanaonyanyasa, wanaowatesa, wanaowadhurumu na kuwagandamiza watu wa tabaka la chini.
Mwandishi katika shairi la “Nikizipata Bunduki ‘’anapendekeza  matumizi ya silaha ili kuondokana na matatizo hayo yote. Hivyo ili tujenge jamii mpya ni lazima tuungane tuwe kitu kimoja kwani  ‘’Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’’.
3. Ujasiri na kujitoa mhanga
Mwandishi anaona ili kuijenga jamii kwa  upya ni muhimu kuwa na ujasiri,kutoogopa vitisho. Katika shairi la “Gorila” ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Gorila,jasiri!
     Wa Afrika ,shujaa,mshupavu,umevinjari,
      Mtutu shika,mevaa,ukakamavu,uko tayari,
      Gorila,ruwaza,wa kizazi kipya
  Mwandishi anaitaka jamii hasa vijana kuwa majasiri na mashujaa katika harakati za kuleta mapinduzi. Pia wanamapinduzi wanatakiwa wawe wavumilivu kwa sababu ujenzi wa jamii mpya sio lelemama, ni safari ndefu.
   Vile vile katika shairi la “Umma”  mwandishi anahimiza ujasiri katika kuleta mapinduzi katika jamii. Mwandishi nasema:-
Umma,
Uliovinjari, kuangamiza  mtabaka,
Hima,
Uwe tayari na usiwena shaka,
Ongoza mapambano,ya wafanyakazi, hadi ushindi.
Hivyo mwandishi anaitaka jamii ijitoe mhanga ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii mpya.
4. Kufanya mageuzi (mapinduzi)
Mwandishi anapendekeza mbinu ya kufanya mageuzi ili kufanikiwa katika suala zima la ujenzi wa jamii mpya. Katika shairi la “Umma” mwandishi anawaasa wanajamii wajiandae kuangamiza matabaka yaliyokithiri katika jamii.
Mwandishi anapendekeza mbinu mbalimbali za kufanya mageuzi (mapinduzi), kwanza, jamii hasa watu wa tabaka la chini waungane ii kuondoa viongozi wanaotumia madaraka waliyopewa kwa manufaa yao binafsi. Katika shairi la  Ungameni” mwandishi anasema;
  Msimamo wa kitabaka,tuwekeni,
 Bepari wote kuwashika,wawe ndani,
 Na mamwinyi bila ya shaka,wambaroni,
 Tusizubae,kazi ianze,twangoja nini?
  Wakati ni huu.
   Pili,mwandishi anapendekeza kutumia silaha katika mageuzi hayo ikiwa unyonyaji hautaondoka kwa amani. Mfano shairi la “Siku Itafika” na “Nikizipata Bunduki” .Pia Katika shairi la “Utawala” mwandishi anapendekeza yafanyike mgeuzi  ili kuuangusha utawala unaojinufaisha na kuendeleza matabaka katika jamii. Katika shairi la “Mjamzito” mwandishi anaonesha jinsi watu wanavyoogopa harakati za mapinduzi katika jamii zetu. Katika mashairi ya “Ni vita si Lelemama” na “Maendeleo ya Umma” mwandishi anaonesha jinsi suala la mageuzi lilivyo gumu, ingawa ana matumaini kuwa umoja na ushirikiano wetu utatufanya tushinde. Pia anaamini kuwa unyonyaji na uonevu hautadumu milele, kwani kuna siku, saa, dakika na nukta itafika uovu wote utaondolewa kwa nguvu.
Katika shairi la “Joka La Mdimu mwandishi anatoa mfano wa tawala dhalimu zilizoondolewa kwa nguvu kwa ushirikiano wa tabaka la chini. Katika shairi hili mwandishi anaonesha jinsi wananchi walivyoshirikiana katika kuutokomeza ukoloni hapa nchini.
Hivyo ili nasi tufanikiwe kujenga jamii mpya hatuna budi kufanya mapinduzi (mageuzi).
5. Kuwa na uzalendo katika nchi
Uzalendo ni ile hali ya kuipenda nchi kwa dhati na hata kuifia. Msimamo wa mwandishi ni kuwa hataihama nchi yake hata kwa kutishiwa njaa, maafa au umaskini. Pia ataipigania nchi yake ili iwe salama. Hivyo hata sisi hatuna budi kuipigania nchi yetu kwa hali na mali ili kuondoa udhalimu uliopo. Katika shairi la  Nchi Yangu”  mwandishi anasema;
 Naipenda nchi yangu,
Naipenda,naipenda nitakufa naipenda.
Tailinda nguvu zangu,tailinda,
Tailinda kwa maafa tailinda,
Sitakwenda kwa wenzangu,
Sitakwenda,sitakwenda hata sifa sitakwenda,
Nitakwenda hku kwangu,nitaganda,
Nitaganda kwa ulofa nitaganda.
   Mwandishi anaona kuwa, tukiwa na uzalendo na nchi yetu tutafanikiwa kujenga jamii mpya, kwani usaliti wa viongozi wetu utaanguka na kila mmoja ataipenda nchi yake kwa  dhati.

6. Kupiga vita ukoloni mamboleo
Ukoloni mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bandia (kisiasa) lakini njia zote za uchumi hutawaliwa au hubaki mikononi mwa mabepari au watu wa nchi nyingine.Katika shairila “Ruya mwandishi anasema;
Ruya,menitoa shamba,mji kuuramba niwe utumwani?
             chini umwinyini,
            nimo kifungoni!
           Ni ‘’huru’’ machoni!
Ruya,hivyo wanitimba,kunifunga kamba,za ukoloni,
         Njozi niondokee!
       Mwandishi anaona kuwa wazungu ndio walioondoka katika ardhi ya Afrika lakini unyonyaji bado upon a unaendelea. Viongozi waliochukua madaraka baada ya uhuru bado wanaendeleza zile taratibu zilizoachwa na wakoloni.
Katika shairi la “Kunguru” mwandishi anaonyesha  pia athari za ukoloni mamboleo hapa nchini. Katika shairi hili mwandishi anazungumzia juu ya kuondoka kwa ukoloni mamboleo. Hivyo mwandishi anaonesha kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita ukoloni mamboleo ili tuwe na uhuru wa kuamua mambo y etu wenyewe.
7. Kupiga vita wizi wa maliya umma
Mwandihi wa diwani hii ameshindwa kuficha hasira yake dhidi ya wizi. Ameutaja wazi kuwa umo kanisani, msikitini, ikuluni na bomani. Waandishi wengi kukwepa kutaja ukweli kama huu. Asemacho mwandishi ni kwamba, sehemu zote za jamii zimeoza. Zamani watu wengi waliamini kuwa viongozi wa dini wana maadili wasiyoweza kuyakiuka. Kwa hiyo, maovu hayo yasingetokea huko. Lakini sasa viongozi hao na wale wa Ikulu wamejiunga na wahalifu. Lililo baya zaidi ni kuwapo kwa “Walinzi” wanaolinda hao wezi.. Shairi hili la “wizi” mwandishi anasema;



Wizi umo;
       Kanisani,
       Msikitini,
       Hekaluni,
Wanyang’anywao ni waumini.
Kwa kifupi wizi umehalalishwa na kubarikiwa .
 Mwandishi  hasemi tufanyeje  Lakini kwa mtiririko na mantiki ya mashairi yake mengine, mwandishi anashauri ufumuaji na usafishaji wa jamii nzima.Katika  shairi la“Kunguru”  mwandishi pia anajadili Suala la wizi . Japo amefumba  lakini anawaelimisha wasomaji kuhusu wezi waliotimuliwa na kutawanywa. Baada ya muda wezi wakajitayarisha kwa mbinu tofauti na kuendeleza wizi wao. Mwandishi  anatanabaisha raia kuhusu kuwapo kwa wezi hawa na marafiki zao. Katika shairi la “Joka la Mdimuni” mwandishi anatanabaisha watu kuhusu uwezekano wa wakoloni kurudi kwa umbo tofauti lakini kwa athari zile zile. Katika shairi la “Naona  Mwandishi anaonesha taabu wanazopata wakulima na malipo duni wanayopewa kwa mzao yao. Anamaliza kwa msimamo huu;
Naona
Ni fukara wakulima
Wamepigwa alitima
Kwa wengine ni neema
Kwao wao ni nakama
Wamekosa haki!
8. Kupiga vita ukasuku wa viongozi wetu
   Mwandishi amekemea tabia za viongozi na watendaji wengine kukubali kila lisemwalo bila kufikiri au kwa hofu tu, si nzuri. Tabia hii ya ukasuku anauita ugonjwa unaohitaji tiba  (tiba yenyewe hakuitaja). Ugonjwa huu hudunisha  akili. Mwandishi anaonyesha  chanzo na athari zake.Katika shairi la “Ukasuku” mwandishi anasema;

Kupea kwa ukasuku
Rais huhubiri
Wabunge hukariri
Wasomi huhariri
Na taifa husimama .
Mwandishi  anawachunguza viongozi wa bara la Afrik na kuwaona kuwa ni mabepari, madikteta, wenye ukabila, wabadhirifu wasiojali raia wao wapenda hongo. Wote amewakemea na kuwakanya wasitende hivyo. Amewapa majina yanayowafaa- wahaini, wasaliti, majasusi n.k. Mwandishi anastahili pongezi kwa kuweza kuwakemea, badhi ya waandishi huwasifu.

UJUMBE
v Uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na kukosekana kwa haki, ukasuku na matumizi mabaya ya mali ya umma ni vikwazo  ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Umoja na ushirikiano ni njia moja wapo ya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mfumo wa ujamaa ni mfumo pekee utakaomkomboa mtu mnyonge, yaani ndiyo utakaoleta hali nzuri kwa wakulima au wafanyakazi.
v Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na ujasiri wa kujitoa mhanga, tuwe wazalendo na nchi yetu na tufanye mapinduzi (mageuzi ya kweli) katika jamii.
v Ukoloni mamboleo ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mapenzi ya kweli ni yale yasiyojali fedha au hali ya mtu.
FALSAFA
Mwandishi anatetea itikadi ya ujamaa yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Analaani wizi, dhuluma na majivuno ya kirasimu. Mwandishi angependa nchi iongozwe kwa haki na usawa. Vile vile anatetea mapenzi ya kweli katika maisha.

MSIMAMO
Mwandisi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani ameonesha matatizo mbali mbali yanayozikumba jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na dhuluma, n.k.
Fani         
a)Muundo
Mwandishi ametumia muundo changamano. Kuna muundo wa tathnia (mistari 2) mfano shairi la “Mjamzito” (uk 5-6), Muundo wa tathlitha  (mistari mitatu) mfano shairi la “Fungate” (uk 1), “Nataka Kusema” (uk 14), Muundo wa tarbia (mistari minne) mfano shairi la “Nahodha Mtwesi” (uk 5), “Gorila” (uk 11), “Afrika” (uk 17) , “Kunguru” (uk 19), n.k.
 Vile vile ametumia muundo wa sabilia au takhimisa (mistari mitano na kuendelea) mfano mshairi ya “Utawala” (uk 21), “Ladha ya Maji Katani”(uk 27), “Joka la Mdimuni” (uk 31), “Mkata “ (uk 15) n.k.
b)Mtindo
Diwani hii ina mashairi yanayofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na yale yanayofuata kanuni za mashairi ya kisasa. Hii ina maana kwamba, mwandishi anayakubali mashairi ya aina mbili (kimapokeo na kisasa)
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi ametumia lugha sanifu yenye lahaja ya Kiunguja. Lugha hii imejaa misemo mbali mbali, tamathali za semi na taswira.
Misemo
Imetumika kwawingi.
Mfano:
i)Nahodha mtwesi chombo chenda joshi (uk 5)
ii)Waja wa Mungu (uk 20)
iii)Paka shume (uk 34)
iv)Utakiona cha mtema kuni (uk 24)
v)Joka la mdimuni (uk 31) n.k.
Tamathali za semi
Tashibiha
Mfano shairi la “Mkata” (uk 15):-
i)Kitandani nilalapo kama dema la samaki…
ii)Mbu ndani kama ndege wa vitani…
iii)Matopeni hujazika mithili nimo karoni…
iv)Nimekoni kama ndizi natokota na kufoka
Sitiari
Mfano shairi la “Uwapi Uzuri Wako” (uk 35)
-Sasa ni chano cha maji, watu wajichanyatia
-Baola mkahawani, kila mtu akaliya
-Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokeya.
Kejeli
-Shairi la “Fungate” (uk 1) linakejeli tabia za baadhi ya viongozi wetu wanaoendelea kuifaidi Fungate ya Uhuru.
-Shairi la “Kantu Sauti ya Kiza”  mwandishi anatumia nyuki kukejeli baadhi ya tabia chafu za watu.
Tafsida
Mwandishi ametumia Tafsida kuyasema maneno makali, machafu, matusi. Mfano shairi la “Paka Shume” linajadili suala la kumendea vitu vya watu kwa njia isiyo halali. Hata neno lenyewe fungate ni tafsida.

Mbinu nyingine za kisanaa
Takriri
Katika shairi la “Mkata” (uk 15), “Dafina” pamoja na shairi la “Nchi Yangu
Mjalizo
Katika shairi la “Mkata” (uk 15).
Mdokezo
Katika shairi la “Mwinyi Mpe Ndiyo”
Ujenzi wa Taswira
Neno Fungate linaleta taswira ya ulimbwende wa maharusi au viongozi. Shairi la “Mjamzito” (uk 5) linajenga taswira ya viongozi waoga katika jamii. Viongozi wasioweza kutatua matatizo ya wananchi. Shairi la “Paka Shume” (uk 34) linajenga taswira ya udokozi. Shairi la “Viongozi wa Afrika” (uk 15) linajenga taswira ya viongozi wanaotumia madaraka  vibaya.
Jina la Kitabu
Kwa ujumla jina la kitabu Fungate ya Uhuru linasadifu  yale yaliyomo ndani ya kitabu. Mwandishi  ameonesha jinsi viongozi wetu walivyo kwenye fungate ya Uhuru. Hali kadhalika wananchi bado wanaendelea kugharamia sherehe mbali mbali za viongozi kwa njia ya michango kama vile kodi, mchango wa mwenge, n.k.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
v Mwandishi amefaulu Kuonesha matatizo mbali mbali ya jamii zetu na mbinu za kuyaondoa.
Kutofaulu kwa Mwandishi
v Mashairi mengi kyanahusu  siasa na hivyo kuwa kama mahubiri ya kisiasa.
v Kusisitiza mfumo wa chama kimoja badala ya mfumo wa mageuzi  na kitabu kiliandikwa  wakati mfumo wa mageuzi umepamba moto dunia nzima.
v Kumfanyia Mwinyi kampeni ni udhaifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa Rais Mwinyi hakuweza kuondoa matatizo aliyoyajadili na ndiyo maana hadi sasa yapo.
v Amekemea uongozi mbaya, lakini hakuonesha chanzo cha uongozi mbaya na mbinu mbali mbali za kuwapata viongozi bora hapa nchini.
v Kutumia lahaja ya Kiunguja ni udhaifu mwingine wa mwandishi, kwani anakinyima Kiswahili sanifu uwanja wa kukua na kuenea.






















KITABU: CHUNGU TAMU
MWANDISHI: THEOBALD MVUNGI
WACHAPISHAJI: TPH
MWAKA: 1985
UTANGULIZI
Chungu Tamu ni diwani iliyoandikwa na  Theobald Mvungi  miaka ya 1980. Katika diwani hii mwandishi anaimulika jamii na kuichunguza kwa makini. Anakosoa na kutoa mapendekezo ili wananchi waondokane na machungu yanayowaandama na kuonja utamu ambao utawafikisha kwenye kheri. Katika diwani hii mwandishi ameonesha dhahiri jinsi Uchungu na Utamu vinayotangamana katika harakati zote za maisha ya mwanadamu. Kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa diwani hii ni kipaza sauti  kinacholia kwa sauti kali kuujulisha ulimwengu juu ya uchungu unaoiandama jamii yetu ya Tanzania .
MAUDHUI
DHAMIRA KUU;  UJENZI YA JAMII MPYA
Suala la ujenzi wa jamii mpya limezishughulisha fikra  za wanafasihi wengi hapa   Tanzania . Jamii endelevu ni jamii mpya ambayo haina ubaguzi, matabaka, uongozi mbaya, yenye kufuata misingi ya haki na usawa. Jamii iliyojikomboa katika Nyanja zote yaani   kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni  na kifikra. Wanafasihi wa Afrika wanaitaka jamii hiyo ijengwe kwa kufuata misingi ya haki na usawa kwa kila mtu. Wameonesha dhahiri kuwa jamii iliyoachwa na wakoloni ilikua imeoza na hivyo zinahitajika juhudi kubwa ili kuondoa uozo huo.
Nchini Tanzania suala la jamii  endelevu  lilianza mara tu baada ya kupata uhuru na kuimarishwa zaidi wakati wa Azaimio la Arusha. Watanzania walitaka wajenge jamii yenye kufuata misingi ya haki na utu, jamii isiyokuwa na matabaka, jamii yenye viongozi waliotakasika, jamii yenye demokrasia ya kweli, jamii isiyo na unyonyaji wa  aina yoyote ile, jamii ambayo hatamu za uongozi zingekuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi, jamii isiyo na dhuluma ya aina yoyote, n.k.
Hadi mwandishia anaandika diani hii anaonyesha kuwa  jamii  bado haijafanikiwa kuifikia lengo la kujenga jamii mpya.
Mwandishi ameonesha  vikwazo  mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya na endelevu hapa nchini na mbinu za kujikwamua kutoka kwenye  vikwazo hivyo.Mwandishi  ametoa mapendekezo ambayo anaamini kuwa endapo jamii itayafuata  itafanikiwa kuijenga jamii  mpya na  endelevu. Mbinu hizo ndizo dhamira ndogo ndogo za diwani hii kama ifuatavyo;
1.      KUPINGA DHULUMA
Dhuluma  ni tendo lisilo la haki, tendo la uonevu, ukatili au uovu. Dhuluma hupingana na haki. Suala la dhuluma hurudisha nyuma maendeleo ya jamii na hivyo ni kikwazo kikubwa cha ujenzi wa jamii endelevu. Suala la dhuluma limemshughulisha sana mwandishi wa diwani hii,katika  shairi la “ Chatu na kuku”  ubeti wa mwisho mwandishi anasema;
Basi  babu akatua akatua,
Funda akajimezea,
Mimi tama imejishikia,
Huzuni imenisaliti,
Kwa chatu kukosa dhati,
Ndipo nikapanga hizi beti,
Ziwe kama ndiyo  hati
Ukumbusho wa huyu dhulumati .
  Katika shiri la “Chatu na Kuku”, mwandishi amelijenga kitaswira kuonesha jinsi wakoloni (chatu) walivyoingia Afrika na kuendeleza dhuluma. Chatu amewakilisha wakoloni na kuku anawakilisha wananchi (Waafrika) walioonyonywa na kudhulumiwa na wakoloni. Mayai ya kuku yanawakilisha mali ghafi waliyodhulumu wakoloni kutoka hapa Afrika.
         Katika shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli”, mwandishi anaonesha jinsi ulanguzi unavyosababisha dhuluma katika jamii. Ameonesha kuwa chanzo cha ulanguzi ni upungufu wa bidhaa muhimu, tamaa, pamoja na uzembe toka kwenye vyombo vya dola. Ulanguzi husababisha  rushwa, magendo na hivyo haki haitendeki katika jamii.
Mwandishi anasema;  
 “Mianzo tukiijua,
Mipango tujipangia,
Kmwe pasiwe na njia,
Ulanguzi kurudia,
Iwe tu twahadithia,
Mithili historia”.
Katika shairi la “Kademokrasia Katoweka”mwandishi anasema;
       Ya msiba atayetamka,
       Udikteta waja haraka,
        Mtemi na walomzunguka,
        Wawatia raia mashaka,
        Dhuluma yatangazwa fanaka.
 Mwandishi anaonesha jinsi wananchi  wanavyodhulumiwa demokrasia yao ya kutoa maoni yao hadharani. Demokrasia inapokosekana, dhuluma ya kutawala kwa mabavu huendelezwa.
   Katika shairi la “Wengine  Wabaki Taabuni”, mwandishi anajadili juu ya dhuluma wanayoiendesha wakubwa dhidi ya watu wa tabaka la chini. Ameonesha kuwa majambazi wanayo idhini ya kufanya kila jambo kwa wanyonge, kwani hayo majambazi hulindwa na wakubwa. Anaendelea kueleza kuwa dhuluma inayoendeshwa na majambazi  hapa nchini ni njama za walinzi (vyombo vya dola).
Anasema;
“Majabazi wanayo idhini,
Kufanya lijalo akilini,
Na hawataingia nguvuni,
Maana walinzi wamo njamani,
Tabu yaanzia kileleni.”
   Mwandishi anaeleza  kuwa tabu inaanzia kileleni maana yake ni tabu au dhuluma inaanzia kwa wakubwa. Hivyo ili tufanikishe suala  la ujenzi wa jamii mpya ni lazima tujitoe mhanga kupambana na kila aina ya dhuluma katika jamii.
2.     KUFANYA KAZI KWA BIDII
Uzembe na kutowajibika ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya jamii yoyote sile. Jamii yoyote ile yenye viongozi wazembe, viongozi wasiowajibika au wananchi wasiojua wajibu wao daima itabaki nyuma kimaendeleo. Mwandishi anaitaka jamii yetu ijue umuhimu wa kazi na kuwajibika katika suala zima la maendeleo. Mashairi kadhaa katika diwani hii yanasisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya jamii. Mashairi haya ni kama vile “Daktari Askari” (UK 11-24), “Chanzo ni Wenye Kauli” (UK 27-28), “Wimbo Wake Hotubani” (UK 28-29) pamoja na lile la “Wengine Wabaki Taabuni” (UK 32-32).
Katika shairi la “Daktari Askari”, mwandishi anaonesha jinsi waganga wanavyojua umuhimu wa kuwajibika katika kazi yao ya utabibu. Ameonesha kuwa wale waganga waliwahudumia majeruhi kwa bidii wakati wa vita. Hivyo kila mtu anatakiwa kuwajibika kama wale waganga ndipo tutaweza kulisukuma mbele gurudumu letu la ujenzi wa jamii endelevu.
Katika shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha utekelezaji na uwajibikaji mbovu unavyosababisha rushwa, magendo na ulanguzi katika jamii yetu. Katika shairi hili mwandishi ameonesha dhahiri kuwa uzembe toka kwenye vyombo vya dola ndio umechangia uwajibikaji kuwa mbovu. Anasema;
“Chombo hiki kuzembea,
Chanzo kilichozidia,
Magendo kuyatetea,
Watu kuwasaidia,
Chombo kilididimia.”
Katika shairi la “Wimbo Wake Hotubani” mwandishi anaonesha utekelezaji  mbaya wa maazimio unavyochangia kuzorota kwa maendeleo ya jamii yetu. Katika shairi hili, mwandishi ameonesha kuwa viongozi wetu wametuna ofisini na shambani hawingii, wanatumia madaraka vibaya, maagizo ni midomoni bila utekelezaji, kila siku-mchana kutwa wanakunywa na kulewa, n.k. Utekeleaji wao uko kwenye hotuba! Mwandishi anasema;
“Cheo kiko mkononi,
Agizo li mdomoni,
Mchana kutwa ndotoni,
Wimbo wake hotubani,
Raia kazi fanyeni.”
Katika shiri la “Wengine Wabaki Taabuni”, mwandishi anaonesha jinsi uzembe kazini, kutowajibika ipasavyo, usaliti pamoja n rushwa unavyorudisha nyuma utekelezaji mzuri wa maazimio tunayojiwekea. Kwa ujumla mshairi anaitaka  jamii ifahamu na kutambua umuhimu wa kazi na wajibu wa kila mmoja katika jamii ndipo tutaweza kufanikisha kuijenga jamii mpya.
I.                   KUWA KIONGOZI MZURI
Suala la uongozi mbaya linaonekana kuwashughulisha sana waandishi wengi wa Afrika. Waandishi wengi wameonesha jinsi ambavyo viongozi wengi walioshika madaraka baada ya mkoloni kuondoka walivyoteka nyara uhuru uliopatikana, kwa hiyo mabadiliko yakawa rangi ya ngozi tu, kwani wananchiwengi waliendelea kuteseka katika umasikini wao.
Nchini Tanzania, pia waandishiwa ushairi kama vile E. Kezilahabi ( Karibu Ndani), T. Mvungi (Raha Karaha na Mashairi ya Cheka Cheka), M.S.Khatibu (Fungateya Uhuru), M.M.Mulokozina K.K.Kahingi (Malenga wa Bara), n.k. wamelijdili suala hili la uongozi kwa mapama sana.
            Mashairi yanayojadili dhana ya uongozi mbaya katika diwani hii ni kama:- “Tishio la Binadamu”, “Chini ya Mti Mkavu”, “Wanajua Kuvumilia”, “Chanzo ni Wenye Kauli”, “Wimbo Wake Hotubani” pamoja na “Shairi la Udongoni”
Katika shairila “Tishio la Binadamu” mwandishi anakemea juu ya uongozi unaotumia mabavu. Mfano mzuri mwandishi anakemea nchi za Urusina Marekani ambazo ni wanachama wenye VETOkwenye umoja wa Mataifa zinavyotumia mabavu kuzikandamiza nchi zisizo na nguvu kisilaha. Mwandish anasema;-
“Kuyasudu mabavu, mwadai tusilotaka,
Maoni yetu chakavu, sawa nguo yamiaka,
Ni pengi penye makovu, nchi zilivyopasuka,
Mabomu yateketeza, waundaji mwafurahi!”
Shairi la “Chini ya Mti Mkavu”mwandishi analaani uongozi unaoendeleza dhuluma katika jamii. Anakemea juu ya uongozi mbaya usiojali maslahi ya wengi, uongozi usiopiga vitaumaskini hapa nchini, n.k.
Shairi la “Wanajua Kuvumilia”, mwndishi analaaniahadi za uongo zinazotolewa na viongozi wetu. Ameonesha kuwa viongozi wetu hawasemi ukweli bali uongo ndio umetawala midomo yao. Sauti ya mshairi inayosikika katika shairi hili lina laani vibaya viongozi ambao hawafiki vijijini kwa wananchi waliowachagua kwa kishindo ili kujionea hali halisi ya maisha wanayoshi. Mwandishi anasema:-
“Afadhali kuimba ukweli,
Wimbo mchomo mkali,
Wimbo, unalilia hali,
Ya vijiji vilivyo mbali,
Kwa wale wasio kauli.”
Katika shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli”, mwandishi anajadili juu ya madhara yaletwayo na uongozi mbaya. Ni dhahiri kuwa chanzo cha ulanguzi, rushwa, uzembe, na kila aina ya uovu ni uongozi mbaya.
Shairi la “Wimbo Wake Hotubani” linjadili na kuonesha jinsi ungozi mbaya unavyochangia utekelezaji mbaya wa maazimio na mipango tunayojiwekea.
Katika shairi la “Kademokrasi Katoweka”, mwandishianaonesha jinsi uongozi mbaya unavyozorotesha demokrasia katika bara la Afrka. Demokrasia inapokosekana udikteta, dhuluma, usaliti, rushwa na kukosekana kwa haki hutawala katika jamii.
“Shairi la Udongoni”  lawakumbusha viongozi wajibu waokatika jamii. Mwandishi anasema:-
“Lanikumbusha wajibu,
Kujenga si kuharibu,
Naahidi kujaribu,
Kulinda tulichojenga.”
Hivyo, ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na uongozi bora. Uongozi mbaya ni kikwazo kikubwa cha ujenziendelevu hapa nchini.
II.                 KUWEPO NA DEMOKRASIA YA KWELI
Demokrasia ni mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu. Demokrasia inahitajika sehemu yoyote ile ili kuwaruhusu wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru bila wasi wasi au kikwazo chochote. Mashairi yanayoongelea suala la demokrasia ni “M janja yu Mashakani”, (UK 25-26), na lile la “Kademokrasi Katoweka”, (UK 30-31)
Katika shairi la “Mjanja yu Mashakani” mwandishi anajadili juu ya mfumo wa demokrasia ambao umejitokeza miaka ya 1980 kote ulimwenguni. Mfumo huu ni ule wa kupiga sera a chma kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi (mageuzi). Katika shairi hili mwandishi anaonesha kuwa mfumo wa vyama vingi umewaamsha wananchi wengi kutoka usingizini na kuanza kutetea haki zao. Hata hivyo, mwandishi anaonesha kuwa wale viongozi waliojilimbikizia madaraka na vyeo mbali mbali wamehofia sana mfumo huu na hivyo hufanya kila mbinu ili kuudididmiza. Viongozi wanaong’ang’ania madaraka ndio wanaohofia mfumo huu. Mwandishi anaonesha jinsi wananchi walivyougomea mfumo wa chama kimoja:-
“Barani migomo baridi, kuugomea mfumo,
Mgomo usokaidi wenye kufumba midomo,
Mfumo uso shahidi , vikao wala misemo,
Ni migomo ya kisiasa, modeli ya kote kote.”
Shairi la “Kademokrasi Kametoweka” linapinga uongozi mbaya barani Afrika.ika shairi hili mwandishi ameonesha kuwa demokrasia inapopokonywa na viongozi wachache, udikteta huota mizizi na kuung’oa huchukua muda mrefu. Hali hii inasababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi barani Afrika. Mfano wa nchi hizo ni Jamuhuri ya Watu wa Kongo, Uganda, Burundi, Sierra Leone, n.k. Utawala wa nguvu hurudisha nyuma maendeleo ya bara la Afrika nan chi nyingine za ulimwengu wa tatu ambako hakuna demokrsia ya kweli. Mwandishi anasema:-
“Barani mabavu yatumika,
Dikteta asijeanguka,
Na majungu pia ayapika,
Udikteta pasi shufaka,
Nasimulia ya Afrika.”
Katika shairi mwandishi anaonesha kuwa mabovu yanatumika ili kumlinda dikteta asije akaangushwa kwa kufuata mfumo wa demokrasia ya kweli. Madikteta hao hutumia vyombo vya dola kama vile polisi, jeshi, magereza na mahakama ili kutetea maslahi yao. Kwa ujumla anatoa pendekezo kuwa, ili tuweze kufanikisha kuijenga jaii endelevu hatuna budi kujenga na kudumisha demokrasia ya kweli katika harakati zetu za maisha.
III.              KUPIGA VITA MATABAKA
Katika kushughulikia suala la mgawanyiko wa jamii katika matabaka ya watu kufuatana na madaraka walionayoya uchumi na siasa, msanii ametumia vielelezo halisi kufikisha ujumbe. Mashairi yanayojadili mgawanyiko wa watu kulingana na hali zao ni kama vile “Chatu na Kuku” (UK 2),  “Wengine wabaki Taabuni”,”Thomasi na Doto” (UK 38), “Wimbo wake  Hotubani” (UK 28), pamoja na  lile la “Manzese Mpaka Ostabei” (UK 43).
Shairi la “Chatu na Kuku” limejengwa kitaswira kuonesha tabaka la wadhulumaji (chatu) na tabaka la wadhulumiwa (kuku). Pia shairi la “Wimbowake Hotubani”linadhihirisha mataaka yaliyopo nchini mwetu. Magavana wanawakilisha tabaka la juu (viongozi) na punda na ngamia wamechorwa kitaswira kuwakilisha wananchi wanyonge wanaoteswa na kunyanyasika. Shairi la “Wengi Wabaki Taabuni” linaonesha kuwa, kuna matabaka ya aina mbili katika jamii- tabaka la wachache wanaofurahia maisha na tabaka la wengi wanaoteseka taabuni. Shairi la “Thomas na Doto” linaonyesha jinsi tabaka la wazungu  (watu weupe) wanavyolibagua tabaka la watu weusi (waafrika), hata katika suala la mapenzi na ndoa. Na shairi la “Manzese mpaka Ostabei” linadhihirisha jinsi mgawanyo wa watu katika matabaka unavyoleta tofauti za maisha katika jamii. Watu wa tabaka la juu huishi sehemu za starehe kama vile Ostabei lakini watu wa tabaka la chini (mafakiri) huishi sehemu duni zenye msongamano wa watu kam vile Manzese, jijini Dar es saam.
Kwa ujumla mwandishi ameonesha kuwa mgawanyiko wa watu katika matabaka huleta utengano katika jamii. Ili tuweze kufaulu kuijenga jamii mpya (endelevu) hatuna budi kupiga vita matabaka yaliyoshamiri katika jamii. Lengo liwe kuijenga jamii . Yenye kufuata misingi ya haki na usawa.
IV.              KUEPUKA VITA (UHASAMA)
Vita husababisha uhasama katika jamii. Huleta ugomvi na kutokuelewana kwa watu. Vita hurudisha nyuma maendeleo ya jamii. Vita huleta athari mbaya katika jamii. Mfano vifo, umasikini, ughali wa maisha, n.k. Mshairi yanayopingana na suala la vita katika diwani hii ni “Tishio la binadamu” na lile la “Daktari Askari.”
Katika shairi la “Tishio la Binadamu”, mwandishi anaitahadharisha dunia kuwa vita kuu vyanukia. Hii ni kutokana na uhasama uliopo kati ya nchi na nchi pamoja na utengenezaji wa silaha kali kutoka Urusi na Marekani. Kutokana na hali hii dunia nzima sasa iko mashakani juu ya vita. Mwandishi anaendelea kueleza kuwa mashindano ya silahayamekuwa ni mchezo nan chi kubwa zinaona fahari kuzitengeneza.  Anasema:-
“Mashindano ya silaha, yamekuwa ni mchezo,
Wakubwa wanaona raha, kwa silaha waziundazo,
Mabomu yaso na silaha, ndiyo yanawapa uwezo,
Urusi na Marekani, dunia mwaipa adha?”
Katka shairi la “Daktari Askari”, mwandishi anaelezea na kusimulia habari za vita kati ya Tanzania na Uganda mwishoni mwa miaka ya 1970. Katika vita hii, Tanzania ilipata hasara kubwa sana kwani uhalifu, ulanguzi, maendo, rushwa vilishamiri wakati wa vita na baada ya vita. Hivyo katika mashairi haya yote mwandishi anaitaka jamii itakayojengwa iepukane daima na suala la vita.
DHAMIRA NYINGINE
I.                   SUALA LA MAPENZI
Mwandishi amejadili aina mbali mbali za mapenzi katika diwani hii. Aina ya kwanza ya mapenzi aliyoyajadili ni yale ya mtu nan chi yake. Haya mapenzi tunayaona katika shairi la “Daktari Askari” ambapo tunona kuwa, wakati wa vita kati ya Uganda na Tanzania raia, wanajeshi, manesi, n.k.walijitolea kwa moyo wa dhati kwenda kupigana ili kuikomboa nchi yao. Mapenzi haya ni ya kweli na dhati. Mapenzi ya Iddi Amina Dada kwa nchi yake hayakuwa ya dhati ndiyo maana alitumia mabavu kuiongoza nchi yake.
Mapenzi mengine kati ya mtu na nchi yake yanapatikana katika shairi la “Ngulu Wapaona” (UK 33-36). Katika shairi hili msanii anaonesha umuhimu wa kuwa na  mapenzi na kwenu (nchi yako) hata kama ni porini. Msaanii anamtaka kila mtu kuthamini kwao ahata kama kuna karaha. Anaonesha kuwa kwenu ni kwenu  na ukuthamini na kukuheshimu kwa raha na Baraka.
Pia kuna mapenzi kati ya mwanamme na mwanamke. Mapenzi haya mwandishi ameyagawa ktika makundi makuu  mawili ya mapenzi ya dhati na yale ya udanganyifu. Mashairi yanayoongelea mapenzi ya dhati ni yale ya “Daktari Askari”, “Thomas na Doto”, “Manzese Mpaka Ostabei” pamoja na lile la “Takumbuka Daima.”  Mashairi yanayoongelea mapenzi ya udanganyifu ni kama vile “Usiwe Mwonja Asali”, “Fikra za Waungwana”.
Mapenzi ya dhati ni  ya kuheshimiana. Mapenzi yasiojali hali au kipato cha mtu. Mapenzi ya uaminifu. Mapenzi kati ya Daktari Adam na Eva katika shairi la “DaktariAskari” yalikua ya dhati, bila kujali kwao au taifa. Hali kadhalika mapenzi kati ya Thomas na Doto yalikua ya dhati bila kujali rangi au taifa. Na mapenzi kati ya Mashaka na Dorothy yalikua ya dhati bila kujali pesa au utajiri. Mapenzi ya dhati husababisha uvumilivu katika maisha. Mapenzi ya dhati huzaa matunda mema katika ndoa, yaani hujenga ndoa za uaminifu. Hivyo mapenzi ya dhati huzaa ndoa za kudumu, ndoa zisizojali rangi, utajiri, utaifa au hali ya mtu. Ndoa za uaminifu zilizotokana na mapenzi ya dhati katika diwani hii ni zile kati ya dakitari Adam na Eva, pamoja na ile ya Mashaka na Dorothy.
Mapenzi ya udanganyifu nayo pia huzaa ndoa za udanganyifu na mara nyingi ndoa hizo huwa hazidumu. Katika shairi la “Usiwe Mwonja Asali”, msanii anaonesha jinsi mapenzi ya udanganyifu yanavyosababish uchumba wa udanganyifu. Pia katika shairi hili msanii anaishauri jamii kuwa ukiwa na mchumba msiwe na tabia za kujamiiana ovyo, bali mpaka mtakapooana. Shairi la “Fikra za Waungwana” linadhihirisha wazi jinsi mapenzi ya udanganyifu yanavyosababisha ndoa za ulaghai. Mwandishi anasema:-
“Mume wangu nakupenda, Joseph amenikuna,
Nimekula naye tunda, ninampenda sana,
Na usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Joseph.”
Katika shairi la “Mfereji Maringo” (UK 57), msanii anawashauri wanajamiikuwa wajiheshimukatika suala zima la mapenzi na wawe waaminifu au wasafi na wasiwe Malaya. Kwa ujumla, katika mashairi haya yote, mwandishianaitaka jamii yetu idumishe mapenzi na ndoa za dhati.
II.                 NAFASI YA MWANAMKE PAMOJA NA UHURU WAKE KATIKA JAMII.
Mwandishi wa diwani hii amemchora mwanamke katika nafasi mbali mbali. Kwanza amemchora kama mwanamapinduzi na jasiri. Katika shairi la “Daktari Askari” mwanamke ameoneshwa akifanya kazi za kimapinduzi sawa na zile za mwanamme. Mwanamke anpigana vita ili aikomboe nchi yake.
Pili, mwanamke amechorwa kama mtu mwenye mapenzi dhati katika jamii. Katika shairi la “Mapenzi Mpaka Ostabei” linamwonesha Dorothy akiwa na mapenzi ya dhati kwa Mashaka . Hali kadhalika katika shairi la “Daktari Askari linamwonesha Eva akionesha mapenzi ya dhati kwa Daktari Adam.
Tatu, mwanamke amechorwa kama kiumbe laghai, asiye mwaminifu hususani katika suala a mapenzi na ndoa. Haya yote tuayoyaona katika shairi la “Fikra za Waungwana”.
Mwisho, mwanamke amechorwa kama mzazi na ezi katika jamii. Katika shairi la “Manzese mpaka Ostabei”, mwanamke amechorwa kama mzazi na mlezi na hii nafasi inawakilishwa na Dorothy ambaye alimzaa motto na kumlea baada ya kuolewa na Mashaka.
Kuhusu uhuru wa mwanamke, msanii ameleta mjadala juu ya uhuru wa mwanamke, uhuru wa kuolewa na wanaume wawili kama afanyavyo mwanaume kwa kuoa wake wawili au zaidi.
Katika shairi la “Fikra za Waungwana” (UK55-57), msanii anajadili dhamira hii kupitia Anna. Katika shairi hili, Anna ana mume wake (Nania) lakini kwa upande mwingine anampenda Joseph mume wake wa pili. Anna haoni sababu ya kutokuwa na wanaume wawili. Kama asemavyo ubeti wa 11:-
“Mume wangu nakupenda, Joseph amenikuna
Nimekula tunda naye, nampendelea sana,
Ila usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Joseph.”
Katika diwani hii, msanii anaonesha kuwa uhuru anaoutaka Anna ni wa kuishi au kuwa na wanaume wawili na huo ndio msimamo wa Anna.
Hata baada ya kesi yake kupelekwa mahakamani, Anna alibaki na msimamo  huo huo. Hali kadhalika majaji walishindwa kutoa hukumu, kwani hakuna sharia inayozui mwanamke kuwa na wanaume wenginkama walivyo wanaume ambao huwa na wanawake wengi.
Lakini swali la kujiuliza ni kuwa, je, mwanamke ana haki ya kuwa na wanaume wawili katika jamii? Hakuna sharia inayomzuia mwanamke kuwa na wanaumewawili lakini mila na desturi ndiyo zinazomzuia mwanamke kuwa na waume wawili. Hivyo ni kutokana na ksoro hizo ndiyo maana anapinga kasoro hizo, kudai uhuru wake wa kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja kama mwanaume anavyooa wake wawili au zaidi kwa wakati mmoja. Hivyo anaishauri jamii kuona inaweka wazi sharia zinazohusiana na suala hili. Majaji walishindwa kuhukumu kesi ya Nania- hii ni kwasababu hakuna kifungu cha sharia kinachomzuia mwanamke kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja.
III.              UMUHIMU WAKUTOA WOSIA
Msanii katika diwani hii anaishauri jamii kutoa wosia kwa familia zao kabla ya mauti kufika. Katika shairi la “Wosia” (UK58-59), msanii anasema kuwa siku yako ikifika, yaani mauti yanapokufikia ni muhimu kutoa wosia kwa familia yako kuhusu mambo ambayo ungetka wakufanyie.
Msanii anatoa wosia wake kuwa yeye akifa jamii inatakiwa imfanyie mambo yafuatayo:-
Kwisha kuniweka chini,
Udongo kasha funika,
Na nyimbo niimbie,
Katoliki yangu dini,
Halafu nawaambia,
Sheree kafanyeni,
Kawaida ya Tanzia (ubeti 2)
Kwa hali hii anaitadharisha jamii kuwa wosia ni kitu cha muhimu kutoa kabla hujafa n sio wosia wa namna watakavyokufanyia, bali hata kuhusu mali zako na namna ya kumilikiwa baada ya kifo chako.
UJUMBE WA MWANDISHI
I.                   Ni lazima tujitoe mhanga ili kutetea wanyonge
II.                 Dhuluma, unyonyaji, kutowajibika pamoja na uongozi mbaya ni baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya.
III.              Mshindano ya kutengeneza silaha kwa mataifa makubwa huhatarisha amani uniani.
IV.              Demokrasia ya kweli ndiyo njia pekee ya kuendeleza mfumo wa mageuzi hapa nchini na katika nchi nyingine za ulimwengu wa tatu.
V.                Mgawanyiko wa watu katika matabaka husababisha kukosekana kwa umoja na mshikamano katika jamii.
VI.              Mapenzi ya dhati yanhitajika katika jamii nan i lazima yadumishwe. Mapenzi ya ulaghai yapigwe vita kwa hali zote.
VII.           Suala la mapenzi na ndoa waachiwe wawili wanaopendana na si maamuzi ya wazazi.
FALSAFA YA MWANDISHI
Mwandishi anaamini itikadi itakavyowatetea wanyonge, yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Analaani wizi, dhuluma, udikteta,unyonyaji na kila aina ya uovu. Vile vile anatetea uhuru katika mapenzi na ndoa.
Mwandishi wa diwani hii ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mali mbali yanazikumba jamii zetu na mbinu za kuondokna na matatizo hyo. Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi mbaya, ulanguzi, dhuluma,rushwa, n.k.
FANI
MUUNDO
Katika ushairi, muundo ni umbo, ploti pamoja na mjengo wa ushairi.Muundo hupatikana kwa kuangalia idadi ya mistari kwa kila ubeti wa shairi linalohusika. Katika diwani hii msanii ametumia miundo changamano. Miundo mikuu iliyotumiwa na mwandishi ni ile ya tarbia (mistari mine kwa kila beti) pamoja na sabilia (mistari mitanona kuendelea kwa kila ubeti).
Mashairi yaliyotumia muundo wa tarbia ni Chungu Tamu” (UK 1), “Tishio la Binadamu” (UK1-2), “Chini ya Mti Mkavu’ (UK 10), “Mjanja yu Mashakani” (UK 25), “Radi ya Kiangazi” (UK32-33), “Shairi la Udongoni”(UK36-37), “Fikra za Waungwana” (UK55-57), “Mfereji wa Maringo” (UK57) pamoja na lile la “Takumbuka Daima” (UK57-58)
Mashairi yaliyotumia muundo wa sabilia ni kama vile:- “Daktari Askari” (UK11-25), “Chanzo ni Wenye Kauli” (UK27-28), “Wimbo Wake Hotubani” (UK28-29), “Wengine Wabaki Taabuni” (UK31-32), “Ngulu Wapaona” (UK33-34), “Chungu na Tamu” (UK34-35), “Usiwe Mwnja Asali” (UK37-38), “Thomas na Doto” (UK38-43), “Manzese Mpaka Ostabei” (UK43-54), pamoja na shairi la “Wosia” (UK58-59). Mashairi mengine yaliyobakia yemetumia muundo wa tarbia kwa baadhi ya beti na nyingine muundo wa sabilia.
MTINDO
Mtindo katika kazi ya fasihi ni mbinu au njia pekee inayotumiwa na waandishi ambayo huweza kumtofautisha mwandishi mmoja na mwandishi mwingine. Katika ushairi, kuna aina mbali mbali za mitindo kama vile mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na mtindo unaofuata kanuni za usasa. Mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo hutawaliwa na urari wa vina na mizani, muwala, mara nyingi kuna mfanano kwa kila kituo, huweza kuimbika, n.k. Mtindo unaofuata kanun za ushairi wa kisasa haufuati au haufungwifungwi na kanuni za ushairi wa kimapokeo. Hakuna urari wa vina, mizani, ufanano wa kituo, kuimbika, n.k.
Diwani ya Chungu Tamu ina mashairi yaliyotumia mtindo changamano, yaani mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na ule unaofuata kanuni za  ushairi wa kisasa. Hii ina maana kwamba, mshairi anyakubali mashairi ya in azote mbili (kimapokeo na kisasa).
Vile vile mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi kwa baadhi ya mashairi. Katika mashairi ya “Chatu na Kuku”, “Daktari Askri” “Thomas na Doto” na “Manzese Mpaka Ostabei”, Mwandishi metumia mtindo huu ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyokusudia.
MATUMIZI YA LUGHA
Aina ya lugha iliyotumika ni sanifu yenye misemo, nahau na methali, tamathali za semi, mbinu nyingine za kisanaa pamoja na ujenzi wa taswira. Lugha ya kishairi yenye uchaguzi maalum wa maneno (diction) imetumika.
MISEMO, NAHAU NA METHALI
Imetumiwa na mwandishi kwa lengo la kuwasilisha ujumbe kwa jamii husika. Mfano:-
a/ Sasa mwaleta shari (msemo) – uk 7
b/ Umoja ni nguvu (methali) –uk 6
c/ Kuvaa masulupwete (msemo) – uk 48
d/ Ndoa ni fumbo (msemo) – uk 42
e/ Usinawe kwa ulimbo (msemo) – uk 42
f/ Mapenzi hayana mipaka (msemo) – uk 40
g/ Utajichimbia kaburi (msemo) – uk 9
h/ Lakini haikutiwa chumvi mitaani (msemo) – uk 12
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
i.Maoni yetu chakavu, sawa nguo ya miaka (uk 2)
ii.Macho yao mekundu mithili wvuta bangi (uk 6)
iii.Kwa msikilizaji husisimua mithili filamu za wachunga ng’ombe
iv.Shaba kama maji (uk 12)
v.Kichwa chake kama cha kifutu (uk 38)
vi.Mwili ukamjaa harara kama jinni lililokosa mbuyu (uk 41)
vii.Tumbo lake kubwa kama pipa (uk 50)
viii.Kichwa kidogo kama cha chatu (uk 50)
ix.Mweusi kama kiatu cha jeshi (uk 50)
x.Utaonekana kama kinyago cha kuchonga (uk 12),n.k.
TASHIHISI
- Kifo kimeniita (uk 4)
-Njaa inawasaliti (uk 6) 
-Kicheche pia ameapa (uk 7)
-Huzuni imenisaliti (uk 10)
-Katika ile baridi kali, mabomu ya mikono, yakatubusu miguuni (uk 16)
-Vichaka vikawakaribisha (uk 38)
-Taa zawaka kwa maringo (uk 44)
-Jiji lasema hali ngumu (uk 44)
-Mapenzi hayana mpango, yakikanywa zaidi, hayana akili ati (uk53)
-Mioto ikapasuka anga (uk 11), n.k.
SITIARI
=Ushairi ni sukari tamu (uk 1)
=Utoto ni kito (uk 2)
=Yeye alisema dunia ni raha na tabu (uk 2)
=Umaskini ni mzigo (uk 11)
=Wote weusi awa mkaa (uk 45)
TAFSIDA
+Usiwe mwonja asali (uk 37)
+Walipenda faragha (uk 51)
+Dora ana kitu tumboni (uk 54)
+Nimekula naye tunda (uk 56)
TABAINA
-Kuwaza na kuwazua
-Lakini usikubali raha tu, kumbuka na karaha (uk 13)
-Aponya aua  (uk 17)
KEJELI
-Nyie yawafalia, mfanyakazi ya kuchoma na kuuza mkaa (uk 45)
-Wa Manzese atakulisha taka (uk 52)
-Jina lenye ugonjwa wa kaka (uk 52)
-Iweje binti shibe aende kwa omba omba (uk 52)
DHIHAKA
-Ati mchumba, mchumba siye Baraka (uk 52)
MBINU NYINGINE ZA KISASA
TAKRIRI
-Mateka, mateka wapenzi (uk 22), Adamu, machozi (uk 20)
-Je je, je….je nyingi (uk 43), Mateka, Mateka, wapewa (uk 22)
-Mama Dora akaasa akaasa (uk 53)
-Tukanyata, tukanyata tukakaribia Mbarara (uk 16)
MDOKEZO
-Je je je…je nyingi (uk 43)
-Si mganga wa tunguli…(uk 14)
-Sijui yaah yaah…(uk 44)
-Sijui Mashaka…(uk 53)
-Kati yao huyu…!(uk 51)
-Profesa Idd Amin…(uk 19)
-Ikawa nakupenda lakini…
NIDAA
-Ati mie mzee1!
-Ghafla mwewe huyu!
-Umeshituka!
-Mwauzunika nini!
-Kwa hamu ya umoja!
TASHTITI
-Hujisikia wezi wakiomba Mungu kabla ya kwenda huko waendako? (uk 13)
-Wewe mwana –kibarua, hujioni? (uk 49)
MJAZIO
-Yule naam, sio huyo, sijui Mashaka…(uk 53)
-Wawaona wanaopelekewa chai, mikate, karanga, mayai…(uk 13)
-Ndugu mwenyekiti nadhani, labda, pengine, ningependekeza, kwa maoni yangu, kwa mfano tungeliweza….(uk 15)
ONOMATOPEA(TANAKALI SAUTI)
-Lo! (uk 4)
-Loooo! (uk 19)
LUGHA YA KIINGEREZA
-Movement order (uk 14)
-Surrender (uk 17)
-Doctor where College? (uk 18)
-Life President? (uk 19)
-Good Doctor (uk 19)
-My first fiancé (uk 20)
-But this is war sir (uk 20)
-Look Adam. My parents are dead. I am alone (uk 23)
-Sir is that a request or an order? (uk 24)
-Two doctors fighting for no reason (uk 25) n.k.
TAFASIRI  YA MOJA KWA MOJA
=Fomu wani (uk 48)
UJENZI WA TASWIRA
Mwandishi ametumia baadhi ya taswira ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyoiandika. Baadhi ya taswira hizo ni kama vile:-
-Chatu (uk 2)…..Inawakilisha wadhulumaji (wakoloni)
-Kuku (uk2)……Inawakilisha wadhulumiwa (Waafrika)
-Vifaranga (uk 9)….Inawakilisha mali ghafi
-Mjanja (uk 25)….Viongozi wanaoshikilia mfumo wa chama kimoja
-Watwana (uk 25)….Wananchi wanaotaka mabadiliko au uongozi mbovu
-Nuglu (uk 33)….Vijiji, sehemu isiyo na maendeleo, sehemu iliyosahaulika
-Zabibu (uk 42)…..Msichana au mwanamke
MANDHARI
Kitbu hiki kiliandaliwa miaka ya 1980. Na matukio yanayosimuliwa katika kitabu hiki yanazungukia nchi za Afrika ya Mashariki hususani Tanzania na Uganda. Hata hivyo, maudhui ya kitabu hiki yanasadifu huu wa sasa katika nchi yoyote ile ulimwengu wa tatu.
JINA LA KITABU
Jina la diwani hii Chungu Tamu linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu. Msanii ameonesha kuwa, baada ya kupita katika machungu na kuamua kupambana nayo ndipo utamu utafuata. Anaitaka jamii itumie kila mbinu kupambana na vikwazo vinavyokwamisha jamii siweze kuupata utamu (ujenzi wa jamii mpya endelevu). Aidha msanii anaonesha kuwa katika maisha, uchungu na utamu havitengamani. Vile vile msanii ameonesha dhahiri kuwa, wananchi wa kawaida ambao ndio wazalishaji wanakula “Chungu” lakini viongozi ambao si wazalishaji wanakula “Tamu”.
KUFAULU KWA MWANDISHI
KIMAUDHUI
·        Ameongelea masuala ambayo yanaisakama jamii yetu katika wakati huu tulio nao. Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala zima la ujenzi wa jamii mpya.
KIFANI
Amefaulu kutumia miundo changamano, mitindo changamano, lugha ya kishairi pamoja na ujenzi wa taswira.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
·        Lugha imejaa taswira kwa kiasi kikubwa na hivyo msomaji wa kawaida hawezi kuambulia ujumbe wowote. Hivyo amewanyima baadhi ya wasomaji uhondo wa kazi yake.
·        Msanii ametumia lugha ya Kiingereza (kigeni) katika baadhi ya mashairi. Huu ni udhaifu wa mwandishi, kwani anakinyima Kiswahili sanifu nafasi ya kuenea. Vile vile kwa mtu asiyefahamu Kiingereza atashindwa kupata ujumbe.   
Na Mwl Godlove  J Gwivaha
 +255 764 745 763
+255 654 407 263
Powered by Blogger.