Dk Kone akemea mila potofu

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Paseko Kone amewaonya wale wote wanaokosoa uumbaji wa Mungu kwa kisingizio cha kutekeleza mila na desturi za makabila yao.
Hayo aliyasema hivi karibuni mkoani Singida katika kongamano la kitaifa la kupiga vita mila potofu ya ukeketaji lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa Linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).
Alisema Mungu alipomuumba mwanamke na mwanaume alikuwa na makusudi yake, kitendo kinachofanywa na baadhi ya makabila kuwakeketa wanawake kwa kisingizio cha kutaka kuwaondolea hamu ya kufanya tendo la ndoa ni sawa na kukosoa uumbaji wake.
“Mungu alikiweka kiungo hicho kwa makusudi yake, inakuwaje sisi binadamu tunaamua kukwangua na kukiondoa kwasababu za kibinadamu,” alihoji.
Hata hivyo, alisema imefika wakati kwa wadau wanaoendelea kutoa elimu dhidi ya mila hiyo kuwaeleza wote wanaotekeleza mila hiyo hoja za kiimani.
“Lazima tutumie hoja zitakazomuingia mtu kiimani, tutafute maneno yatakayowagusa katika imani zao yatakayowafanya waachane na vitendo hivyo, tusimkosoe Mungu kwa kisingizio cha kutekeleza mila,” alisema Dk Kone.
Powered by Blogger.